Karibu sana rafiki yangu kwenye blog yako ya mshindi.
Kamwe kwenye maisha yako usisahau wewe ni baharia wa meli yako.Jambo la kuwa kiongozi wa Maisha yako ndilo linalokufanya uhitaji kujifunza kila siku ili uweze kukua zaidi.
Baharia kipindi anajifunza kuiendesha meli lazima ajifunze kuyazoea mawimbi ya maji.Azoee hali mbalimbali za mabadiliko ya hali ya hewa.Awe na tahadhari kwa matukio yanayoweza kutokea bila ya kutarajia.
Kama ilivyo kwa maisha ya baharia,ndivyo ilivyo pia kwenye maisha yetu.Utakutana na vikwazo mbalimbali kwenye safari ya maisha yako.Yawezekana ukawa na mipango mingi mizuri lakini ikaharibika,na viko vitu vingi vinavyoweza kutokea nje ya udhibiti wako.
Kwa vyovyote vile ,matarajio aliyonayo baharia ni kuifikisha meli yake bandarini kwa usalama.Iwe anaogopa mawimbi au la inamlazimu kupambana kuhakikisha anatimiza jukumu lake kwa ufasaha.
Nini kinamfanya baharia kuwa imara,zidi ya mawimbi makubwa ambayo muda wote huiiyumbisha meli?jibu ni moja tu ni mbinu mbalimbali alizo nazo za kukabiliana na hali inayojitokeza.Ukubwa wa mawimbi haumfanyi baharia kuacha kuendelea na safari yake.
Ni kweli kabisa wakati mwingine anaweza kuogopa kufa,lakini kwa kuwa anaijua kazi yake,anaamua kupambana.Anajua kukimbia kuiongoza meli yake zidi ya mawimbi hayo hakutasaidia chochote.Anafahamu bila kupambana na kuielekeza meli yake vyema chochote kinaweza kutokea na kuizamisha meli yake haraka.Hivyo anajua vyoyote itakavyokuwa lazima apambane zidi ya dhoruba yoyote.
Vivyo hivyo kwenye maisha yetu ya kila siku,Kuna kupitia dhoruba mbalimbali.Ni muhimu kujifunza mbinu za kukabiliana na chochote kinachoenda kutokea,vinginevyo dhoruba hizo zitatushinda na tutakuwa tumeanguka kabisa.
Baharia mwoga au yule anayejiona anaweza kuwa na bahati mbaya yeye huwa anasubiria mpaka kipindi bahari inapokuwa na utulivu,ndipo anapoweza kwenda na inapotokea dhoruba isiyotarajiwa hushindwa.
Baharia imara huwa hamlaumu yeyote bali yeye binafsi,na hujifunza kupitia makosa yake,na ikitokea kipindi kingine cha dhoruba yeye huhakikisha anashinda.Anajua kilichomkwamisha hapo awali ni upungufu wa mbinu alizokuwa nazo.Hivyo huamua kwenda kwa mabaharia wengine na kujishusha ili kujifunza mbinu wanazotumia wenzake .Anapojua vyema hurudi na kuendesha meli yake mwenyewe.
Haya ninayokueleza hapa usijisahau ukafikiria nilikuwa nakuhadithia habari za mabaharia wa meli au maboti.Hapana,hapa ninachokuelezea hapa ni habari ya wewe na maisha yako.
Na Kama hujui nini cha kufanya ni muhimu kuwatafuta watu watakaokufundisha jinsi ya kufanya hadi na wewe uweze kufanya mwenyewe.Kwa vyovyote vile fanya vile vitu vitakavyokufanya kuwa baharia kwa meli yako mwenyewe.
Unayaangalia maisha yako na unajiona unaweza kuwa mshindi.Lakini lazima uwe Kama yule baharia imara ili uweze kuwa mshindi.Haijalishi ni kwa kiasi gani unaihofia safari yako,bali kinachotakiwa ni kwa namna gani unaweza kupambana ili kuishinda hofu yako na kusonga mbele.Fanya miugiza itokee,haijalishi ni dhoruba gani imekupata kwenye maisha yako.Wewe jiandae na uwe na mbinu mbalimbali za kuibuka mshindi.
Mwandishi wa makala hii ni Emanuel mcharo barua pepe ni mcharoima@gmail.com.