USHINDI NI LAZIMA KWAKO USIKATE TAMAA:

Inawezekana uko kwenye hali ngumu, na unafikiri hakuna tena tumaini. Ni kweli inaweza kufikiriwa hivyo. Lakini pale unapotambua kuwa Unatakiwa uwe kwenye hali nzuri, unapata nguvu kubwa ya kupambana.

Tuchukulie umeteguka mguu, na akatokea mtu anakuambia kimbia. Utaanza kujitetea jinsi gani huwezi kukimbia,na hata watu wanaweza kukutetea kulingana na hali wanayokuonanayo.

Lakini hapo hapo katikati ya mabishano ya kwanini huwezi kukimbia, akatokea mtu mwenye bunduki na anataka akue utashangaza watu kwa kasi utakayokimbia. Unapata nguvu kubwa pale unapojua uhai ni muhimu kuliko maumivu ya kuteguka.

Kule kujua Unatakiwa kuwa hai kunakupa sababu ya kuyashinda maumivu. Ni kweli ilionekana huwezi kukimbia, lakini hilo haliwezi kukufanya umsubiria yule mwenye bunduki akufikie ulikuwa umekata tamaa ya kukimbia.

Kwa vyovyote vile utafanya jitihada za kujiokoa. Kule kuhisi kukosa matumaini ni njia iliyotengenezwa ili ujihisi wewe ni mnyonge lakini sivyo ulivyo hata kidogo. Unakuta jengo la ghorofa za juu linawaka moto,na watu wanaokoa maisha yao kwa kuruka. Miongoni mwa watu utakaowaona wakiruka kutoka juu ni wale waliofikiriwa hawataweza kuruka. Watu huruka na sababu ni kutafuta ushindi.

Uwe na matumaini ya ushindi kuliko kung’ang’ania kukata tamaa. Unapokuwa na matumaini ya kuwa hai ndipo unapopata fursa ya kushinda vizuizi vilivyopo mbele yako. Hakuna hali mbaya kama utakuwa na uwezo wa kuendelea kujaribu. Na uamini chochote kinaweza kutokea huko mbele ya safari.

Timu ya mpira inaweza kufungwa magoli 3 mapema. Lakini wachezaji huendelea kupambana hadi dakika ya mwisho. Utashangaa kuiona timu iliyokuwa imefungwa goli 3 ikiibuka na ushindi wa 4-3 kwenye dakika za mwisho.

Mashabiki wa timu iliyotangulia kufungwa walivyoona dakika zilizobakia walikata tamaa ya timu yao kushinda. Wengi walianza kuondoka uwanjani, wale wa majumbani walibadilisha channel za runinga zao, wale wa redio walizima redio zao. Lakini katika kipindi hicho kidogo timu yao ilibadilika na kuleta matokeo yasiyotarajiwa ya kushinda goli 4-3. Chochote unachopitia kama uko hai amini ushindi upo. Siri ya washindi ni kubakia kwenye mchezo hadi dakika ya mwisho.

Mwandishi wa makala ni Emanuel mcharo. Barua pepe mcharoima@gmail.com

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started