Changamoto zile tunazopitia,ndiyo zenye uwezo wa kutufanya tukue.

Kile kinachoendelea kukuzunguka kwenye maisha yako kisiwe kikwazo kwako. Pale unapoenda baharini, unaweza kuyaona mawimbi maelfu kwa maelfu.

Lakini kwenye vilindi vya bahari hiyo kunakuwa na utulivu na ukimya mkubwa. Mawimbi yote huonekana kwenye uso wa bahari tu.

Zama ndani yako kwa tahajudi na sala, maana mahangaiko na misuguano ni kwa nje tu, ndani yetu kunao ushindi mkubwa ambao hauwezi kufikiwa na yale yanayotuzunguka.

Kama ilivyo kwenye vilindi vya bahari visivyoweza kufikiwa na mawimbi basi ndani yetu hakuwezi kufikiwa na kile kinachotusumbua kwa nje. Iwe umasikini, ugonjwa nk. Tuyachukulie maisha yetu Kama majaribio ya kisayansi.

Wanasayansi wako imara sana ndani yao. Pale wanaposhindwa jaribio la kiutafiti, hawakati tamaa bali hutumia kushindwa huko kama kituo cha kuwaongoza kwenda kwenye mafanikio.

Jiulize ni majaribio mangapi wameyafanya na kuanguka kwenye kupata dawa ya kuutibu ukimwi? Ni majaribio mangapi yamefanyika kwenye ugonjwa wa uviko 19.

Kumbuka wanasayansi wanatumia kila anguko kama kituo muhimu kwao kinachowasaidia kusonga mbele.

Sisi pia tunatakiwa kuwa kama wanasayansi,kutumia kila anguko tunalopata kama sehemu ya kusonga mbele. Na tusiruhusu kile kinachotuzunguka kwa sasa kuwa kikwazo,bali tukitumie kama kituo cha kuendelea mbele.

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started