MAISHA NI NINI?

Maisha ni kuumba. Unaweza kuipata maana halisi ya maisha yako ikiwa utaamua kuitengeneza maana hiyo. Maisha ni kama shairi linalosubiria kutungwa.

Maisha ni wimbo unaotakiwa uimbwe, ni mziki unaotakiwa uchezwe. Maisha kama maisha hayana maana, maisha ni fursa ya kutengeneza maana.

Maana hiyo haitakuwa kitu kinachotakiwa kuvumbuliwa. Bali maisha ni kitu kinachotakiwa kiundwe. Maana ya maisha unaweza kuipata kwa kutengeneza aina ya maisha yale unayoyahitaji.

Maisha siyo kitu unachoweza kuzunguka nyumba na kukutana nacho. Au useme ni kitu kilichopotea ukikitafuta kidogo utakipata. Maisha siyo madini, useme ukiyachimba utayakuta. Maisha halisi ni kama mashairi yanayotakiwa yatungwe.

Maana ya maisha ni kucheza mziki na siyo kukutana nao. Huwezi kukutana na mziki, na maana ya mziki ni ucheze.

Maana utakayoipata kwenye maisha yako ile tu uliyoitengeneza, na hilo ndiyo jambo la muhimu kukumbuka.

Wengi wetu tumekwama kwa kuwa tunafikiri maisha ni kitu kinachopaswa kuvumbuliwa, kama kitu hicho kilikuwepo tayari.

Watu wanafikiri maisha ni kama kupasua mwamba na kuyakuta madini. Maisha hayana maana hiyo kwamba paa kitu kimetokea kiko hapa. Utawakuta vijana wa siku hizi wakisema one day yes. Wakifikiri ipo siku maisha yenyewe yatatokea kama dodo chini ya mwembe.

Kumbuka hakuna maana nyingine ya maisha zaidi ya ile uliyoitengeneza. Ukiona Kuna maana yoyote kwenye maisha yako ni sababu wewe unahusika kuitengeneza.

Mungu siyo kitu zaidi ya mwumbaji. Na yeyote anayetaka maana ya maisha anatakiwa ayaumbe.

Maisha siyo kitu kilicholala sehemu fulani. Siyo kitu kinachohitaji kuvumbuliwa. Kama ingekua ni kitu kinachohitaji kuvumbuliwa basi mtu mmoja angetosha kuvumbua. Na kusingekuwepo na haja ya kumta kila mtu avumbue. Kwa kuwa maisha ni kuumba basi kila mtu lazima aumbe maisha yake anayoyataka. Na kule kuumba maisha yako ndiko kunakoyapa maisha maana.

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started