Kila unapopanda daraja la juu kwenye maisha yako, waheshimu wale walio kwenye daraja la chini. Maana uliyo juu leo tambua kuna watu waliamua kukubeba kwenye mabega yao.
Leo unaweza kuona mbele, kwa kuwa uko kwenye mabega ya watu walioamua ukanyage mabega yao. Waheshimu sana watu hao maana wakikususa, lazima utajikuta chini na huo ndiyo utakuwa mwisho wako wa kuangalia mbele kwa kutumia mabega yao.
Siku zote awali ni awali tu hata kama ulipata kidogo bado ndiyo kinayobakia msingi wako. Mwanafunzi wa chuo anaweza kumdharau yule mwalimu aliyemfundisha chekechea. Lakini kiuhalisia anabakia yule mwalimu wa chekechea ndiye aliyemfungulia njia yeye kuweza kukutana na profesa huko kwenye elimu yake ya juu.
Jiulize kama huyo aliyekuonyesha njia awali, angekujengea njia mbovu leo huko juu ungefika?
Lakini hilo la wewe kuwa na elimu kubwa kuliko mwalimu wako wa awali siyo kosa. Maana kulingana na viwango vya maisha ndiyo huamua, pale unapotaka cha juu lazima ukubali kutapoteza kile kilichoko chini yako.
Pale unapoondoka kwenye daraja la chini na kwenda juu, lazima kuna watu utawaacha ili usonge mbele. Na unapoamua kusonga mbele huna haja ya kugombana na mtu au kumdharau yeyote. Ni safari ya muda tu, mnaweza kutoka wote kijijini kwa kutembea kwa miguu. Lakini mkifika kituo cha usafiri kila mtu huchagua usafiri wake.
Naamini umenunua viatu ili vikusitiri miguu yako.
Pamoja na nia yako ya kutaka viatu hivyo vikusitiri, ukifika sehemu yenye matope inakubidi uvivue na kuvibeba.
Unajikuta ile nia yako ya kusitiriwa na viatu inageuka wewe kuvisitiri viatu hivyo.
Kuna kuwa hakuna namna nyingine ni kupambana na hali yako. Unaanza kujiuliza maswali, je niingie na viatu hivi kwenye tope? Au niingie mimi peku nikitoka salama nivirudie viatu vyangu na kuendelea na safari.
Kile utakachokiamua ndiyo kitaamua safari yako iweje.ukiamua kuzamisha viatu kwenye tope ujue hapo ni mwisho wa kuendelea navyo kwenye safari yako.
Uamuzi wote uko juu yako.
Na safari hii ya viatu haina tofauti na safari tuliyonayo kwenye maisha yetu ya kila siku.
Kuna watu watakuwa na wewe kwenye hali fulani, lakini hawa ukifika kwenye matatizo fulani hawatakufaa tena. Utaingia mwenyewe kwenye matatizo yako huku wakitaka wewe uwasaidie.
Hivyo Unatakiwa kujua baadhi ya marafiki, urafiki wao ni kama wa viatu. Pale njia ikiwa nzuri viatu vyako viko na wewe, lakini hali ikibadilika ndiyo mwisho wa urafiki wenu.
Maana Kama utalazimisha viatu vyako uingie navyo kwenye tope basi ujue vitanasa au vitachanika na kuharibika kabisa. Ukiwa na busara lazima uvivue na uvibebe , sasa vimekuwa mzigo juu yako.
Na hili ndiyo somo tunalotakiwa kujifunza, kwamba siyo kila rafiki, utakayekutana naye ataweza kukuvusha kwenye kila changamoto.
Kuna kipindi yule uliyemtegemea atageuka kiatu na inakupasa kumvua na kumweka pembeni ili maisha yaendelee.
Siyo vibaya wewe kuwaweka pembeni baadhi ya marafiki zako ambao wanageuka mzigo. Uking’ang’ana nao utakwama na kuchafuka na huo utakuwa mwisho wa safari yako.
Unapoifikia changamoto kubwa, pambana na hali yako, na tafuta marafiki wenye uwezo wa kuimudi hiyo changamoto unayoipitia. Tafuta wale unaweza kuvuka nao ng’ambo. Na waheshimu wale uliowaacha wakiendelea na maisha yao bila wewe kuwatusi au kuwadharau.